
_Utanufaisha Kata 7, Kata mbili za Kemondo na Bujugo zimeanza kupata maji, Rais Samia apania kumtua Mama ndoo kichwani._
Naibu Waziri wa Maji Eng. Kundo Mathew amefika kwenye Tarafa ya Katerero iliyopo Bukoba mkoani Kagera kukagua mradi mkubwa wa Maji wa Kemondo- Maruku unaogharimu Bilioni 15.8 ukiwa kwenye Kata ya Kemondo huku chanzo chake cha maji kikiwa ni Ziwa Victoria. Mradi utanufaisha zaidi ya wananchi 100,000 (Laki moja) wa Kata 7 na sasa Kata mbili za Kemondo na Bujugo zimeanza kupata maji.
Naibu Waziri alitembelea na kukagua kiosk na chanzo cha maji eneo la Ziwa Victoria palipojengwa pampu mbili kubwa za kisasa zinazosukuma maji kutoka Ziwa Victoria pamoja na kukagua tenki kubwa la maji lenye ujazo wa Lita Milioni 3 linalopokea maji kabla ya kusambaza kwa wananchi.
Tenki kuu la maji la Lita milioni 3 la mradi huu linatajwa kuwa moja ya tenki kubwa za maji mkoa wa Kagera ambapo Naibu Waziri Kundo alipanda juu ya tenki na kulikagua vyema lote na kusema limekamilika kwa asilimia 100 ikiwemo mifumo yote ya pampu na miundombinu yake huku akisisitiza ni dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan kusukuma mradi huo na mingine mingi inayotekelezwa nchini ili kumtua Mama ndoo kichwani na wananchi kwa ujumla kupata maji na salama.
Mradi wa Maji Kemondo ni moja ya miradi mikubwa itakayonufaisha takribani Kata 7 za Kemondo, Katerero, Bujugo, Kanyengereko, Maruku, Muhutwe na Mayondwe huku Kata mbili za Kemondo na Bujugo zikiwa zimeanza kupata maji. Serikali ya Rais Samia inautekeleza na kuukamilisha baada ya kuombwa na Mbunge wa Bukoba Vijijini Mhe. Jasson Rweikiza wakati wa Uongozi wa Serikali ya Awamu ya 5 iliyokua ikiongozwa na Hayati John Pombe Magufuli na sasa Serikali ya Rais Samia inaukamilisha.
Naibu Waziri Kundo kwenye ziara hiyo aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Bukoba Mhe. Erasto Sima na Kamati yake yote ya Usalama ya Wilaya, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Bukoba Vijijini Bi. Fatina Laay, Wataalamu wa Maji kutoka RUWASA, BUWASA, Afisa Tarafa wa Tarafa ya Katerero Ndugu Bwanku M Bwanku, Viongozi wa CCM Kata, Diwani wa Kata ya Kemondo Ndugu Khatwibu Kahyoza, Mtendaji wa Kata Ndugu Cyriacus Sosthenes na wengine wengi.