
_▪️Ni katika siku ya Tanzania kwenye maonesho ya Osaka World EXPO 2025_
_▪️Asema mauazo ya bidhaa za Tanzania Japan yafikia sh bilioni 37_
_▪️Asisitiza Tanzania ni mahali salama kwa uwekezaji_
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema ushirikiano wa Tanzania na Japan umezidi kukua katika nyanja za kiuchumi, kisiasa na kidiplomasia umezidi kuimarika siku hadi siku, ambapo mauzo ya biashara kati ya nchi hizo yameongezeka kutoka dola za Marekani bilioni saba mwaka 2023 hadi bilioni 37 kwa mwaka 2024.
Mheshimiwa Majaliwa ameyasema hayo leo (Jumapili, Mei 25, 2025) alipomwakilisha Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati wa maadhimisho ya Siku ya Tanzania kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Osaka (World Expo Osaka 2025) yanayoendelea nchini Japan.
Amesema Wajapan wanapenda sana bidhaa kutoka Tanzania zikiwemo za kilimo kama chai, kahawa, ufuta, tumbaku, tingatinga, vinyago, katani, viungo kama karafuu pamoja na madini mbalimbali yanayopatikana nchini.
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji na wafanyabiashara wa Japan na duniani kote waje kuwekeza katika maeneo mbalimbali nchini yakiwemo ya elimu, afya, miundombinu, nishati, kilimo, utalii kwani Tanzania imeweka mazingitra mazuri ya uwekezaji na pia ina amani na utulivu.
“…Tanzania licha ya kuwa na fursa nyingi za uwekezaji ikiwemo ardhi yenye rutuba, amani na mazingira tulivu, pia ni kitovu cha biashara katika Ukanda wa Afrika Mashariki, Kusini na Kati kwa kuwa inapakana na nchi saba ambazo ni Uganda, Rwanda, Burundi, Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Zambia, Malawi na Msumbuji hivyo kuwawezesha wawekezaji kupata masoko ya uhakika katika mataifa hayo.”
Waziri Mkuu amesema Serikali ipo katika mchakato wa kuvifanyia maboresho viwanja vya Maonesho vya Mwalimu Julius Nyerere maarufu sabasaba ili viwe na hadhi ya kimataifa na kuwezesha kufanyika mikutano na maonesho ya biashara ya kikanda na kimataifa.
Monesho hayo yamehudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanziba wakiwemo Mawaziri, Manaibu Mawaziri, Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu na Wakuu wa Taasisi mbalimbali.
Maonesho hayo yalianza tangu Aprili 13, 2025 na yanatarajia kumalizika Oktoba 13, 2025, hii ni mara ya pili kwa Japan (Osaka) kuwa mwenyeji wa maonesho hayo ya kimataifa, ambapo mara ya mwisho yalifanyika 1970 (EXPO 1970).
Kesho (Jumatatu, Mei 26, 2026), Mheshimiwa Majaliwa anatarajiwa kushiriki katika kongamano la biashara, uwekezaji na utalii ambalo litahusisha wafanyabiashara kutoka Tanzania na Japan. Pia, Waziri Mkuu atashiriki katika Mikutano ya Uwili na viongozi wa Serikali ya Japan, mashirika ya maendeleo na watendaji wakuu wa makampuni mbalimbali kwa lengo la kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Japan.