
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule ameahidi kuwa Serikali ya mkoa wa Dodoma itaendelea kushirikiana na Makao makuu ya Mahakama ya Tanzania yaliyopo Dodoma katika kuhakikisha kuwa dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan inatimia katika kuhakikisha wananchi wa Tanzania wanapata haki zao.
Mhe. Senyamule amebainisha hayo leo Aprili 05, 2025 wakati Rais Samia akishiriki kwenye uzinduzi wa Jengo la Makao makuu ya Mahakama kwenye eneo la Tambukarelo Mjini Dodoma. Akiwakaribisha Dodoma watendaji wa Mahakama wakiwamo Majaji wa Mahakama ya Rufaa ambao tayari wamehamia Mkoani Dodoma na hivyo kukamilisha Mihimili mitatu kuwa na makao makuu Dodoma ambayo ni Serikali, Bunge na mahakama ya Tanzania.
Mhe. Senyamule pia amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa utashi wake anaoendelea kuonesha kwa Watanzania, akisema Rais Samia Hajavunja rekodi bali ameandikisha historia mpya Tanzania kwa kutekeleza na kujenga miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo imekuwa chachu ya ustawi wa watanzania.
Akizungumzia Jengo la Mahakama lililozinduliwa leo, Mhe. Senyamule ameeleza kuwa jengo hilo si tu la mahakama bali pia ni utalii na uchumi wa Mkoa wa Dodoma kwani anaamini litakwenda kuongeza mzunguko wa uchumi kutokana na mwingiliano wa watu utakaoongezeka Dodoma pamoja na kuwa kivutio cha utalii kutokana na upekee wa jengo hilo ambao haupo nchini wala kote barani Afrika.