9 views 4 mins 0 comments

ZIMAMOTO YAUNGANA NA MATAIFA MENGINE KUADHIMISHA SIKU YA WAZIMAMOTO DUNIANI

In KITAIFA
May 04, 2025



Na Mwandishi wetu – Dar es Salaam

Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Tanzania Bara, limeungana na Wazimamoto  wote Duniani katika kuadhimisha Siku ya Wazimamoto Duniani ambayo hufanyika Mei 4, kila mwaka.

Akizungumza na Waandishi wa habari Mei 04, 2025 jijini Dar es Salaam Naibu Kamishna wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji (DCF) Puyo Nzalayaimisi, ambaye pia ni Msemaji wa Jeshi hilo amesema kuwa siku hii ilianzishwa rasmi mwaka 1999 kufuatia tukio lililotokea nchini Australia ambapo wazimamoto watano walifariki wakijaribu kuzima moto katika msitu uliopo eneo la Linton Jimbo la Victoria.

Tukio hili liliamsha hisia kwa Wazimamoto wote Duniani na kuamua kuwakumbuka na kuwaenzi kwa kuweka azimio la kuwakumbuka mashujaa wote waliopoteza maisha wakitekeleza majukumu yao kwa kuanzisha Siku ya Zimamoto Duniani.

Aidha, Maadhimisho haya yanatambua mchango Mkubwa wa Maafisa na Askari wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji katika kulinda maisha na mali za wananchi dhidi ya majanga mbalimbali yakiwemo ya Moto, matetemeko ya ardhi, Mafuriko, maporomoko ya ardhi, ajali za barabarani na majanga mengine.

Amesema katika nchi ya Tanzania kumeshuhudiwa matukio makubwa na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji likionesha weledi, ushujaa na uzalendo mkubwa na miongoni mwa hayo ni lile la watu kuzama katia Ziwa Rukwa Januari 2025, maporomoko ya matope Hanang Manyara Disemba 2023, Mafuriko Rufiki Pwani Aprili 2014, Kuporomoka kwa Jengo Kariakoo jijini Dar es salaam, moto katika Misitu ya Mlima Kilimanjaro Oktoba 2022 na 2020, moto wa misitu ya Sao Hill Mkoani Njombe Novemba 2024.

Miongoni mwa majanga mengine ni pamoja na Ajali ya Treni na Basi Mkoani Singida Novemba 2023, Moto wa Matanki ya mafuta Kigamboni Januari 2020, Moto wa Lori la mafuta Mkoani Morogoro Agost 2019, Moto wa TIPPER mwaka 1999, Benki Kuu 1984, Moto wa Ubungo 2004, na majanga mengine ambapo Maafisa na Askari walijitolea kwa ujisiri mkubwa kuchukua hatua za haraka kuokoa maisha ya Watanzania.

Naibu Kamishna Nzalayaimisi amesema miongoni mwa malengo ya maadhimisho ni pamoja na kutoa heshima kwa Wazimamoto waliopoteza maisha wakiwa kazini, kutambua mchangango wa wazimamoto walioko hai katika jamii, kuelimisha Umma kuhusu majukumu ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji hatua ya tahadhari, kujenga uhusiano wa kimataifa kati ya vyombo vya Zimamoto na Uokoaji pamoja na kutoa Motisha kwa Wazimamoto kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa moyo wa uzalendo.

Amezitaja pia baadhi ya shughuli ambazo Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limeshiriki kuanzia wiki ya Maadhimisho haya mpaka hii leo ambapo ni siku ya kilele ni pamoja na usafi katika Hospitali na Vituo vya Afya na maeneo mengine, uchangiaji damu wa hiari kwa ajili ya wahitaji, utoaji wa misaada ya kibinadamu katika Magereza na Vituo wanavyoishi watu wenye uhitaji maalum, utoaji elimu kwa umma kuhusu kinga na tahadhari dhidi ya moto katika shule, masoko, vituo vya usafiri, mikusayiko ya watu kupitia vyombo vya habari.

Hata hivyo ametoa Pongezi na shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuliwezesha Jeshi hilo katika kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kutambua mchango mkubwa wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, wananchi wanoshirikiana na Jeshi kwa kutoa taarifa haraka pindi majanga yanapotokea.

Aidha siku ya Wazimamoto Duniani si siku tu ya kumbukumbu bali mwito wa mshikamano, uzalendo na kuthamini thamani ya maisha ya binadamu.

/ Published posts: 1989

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram